I made this widget at MyFlashFetish.com.

Friday, September 3, 2010

RAIS KARUME ATEMBELEA UJENZI WA BARA BARA KISIWANI PEMBA

AIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dk. Amani Abeid Karume ametoa pongezi kwa Idara ya Barabara Pemba pamoja na wananchi wa Mtambile,Kangani, Kengeja na Mwambe kwa kushiriki vyema katika ujenzi wa barabara zinazopita vijijini mwao.

Rais Karume alitoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti wakati alipokuwa katika ziara ya kutembelea ujenzi wa barabara za Mtambile-Kangani na barabara ya Mtambile,Kengeja-Mwambe Kisiwani Pemba.

Katika ziara yake hiyo Rais Karume alitoa pongezi kwa wananchi wa maeneo hayo ambao wamekuwa wakishiriki kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa barabara ikiwa ni miongoni mwa barabara zilizomo kwenye Mradi wa Barara za vijijini Kusini Pemba.

Rais Karume aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuongeza juhudi zaidi katika shughuli hiyo ya ujenzi wa brabara ambapo wananchi hupata ajira kwa kiasi kikubwa kutegemea na juhudi zao za kazi.

“Shukrani kwa msaada na mchango wenu mkubwa katika ujenzi wa barabara hivyo ongezeni juhudi na nguvu ili mpate kuendelea na ujenzi kwa ufanisi mkubwa”,alisema Rais Karume.

Akitembelea ujenzi wa barabara hizo ambazo kwa asilimia kubnwa ujenzi wake umekuwa ukiwashirikisha wananchi wenyewe, Rais Karume alisifu juhudi za wananchi hao.

Nae Muhandisi Mkaazi wa Idara ya Barabara Pemba, Khamis Masoud alimueleza Rais Karume kuwa kazi zinaenda vizuri na kuna matumaini makubwa ya kumaliza kwa wakati na kwa ufanisi zaidi.

Masoud alisema kuwa barabara hizo ni miongoni mwa barabara 6 zenye urefu wa kilomita 44.7 ambazo zimo katika Mradi huo wa Barabara za vijijini Kusini Pemba.

Alisema kuwa kazi nyingi za mwanzo katika ujeni huo zimeshalkuwa tayari kwa upande wa barabara ya Mtambile-Mwambe yenye urefu wa kilomita 9.4 ambapo tayari kilomita 2 zimeshaaza kutiwa lami.

Aidha, Masoud alisema kuwa kwa upande wa barabara ya Mtambile-Kangani yenye urefu wa kilomita 6.4 nayo kazi zake za ujenzi zinaenda vizuri. Pia, alisema kuwa barabara ya Miingani-Wambaa yenye urefu wa kilomita 9.7 nayo imo kwenye mchakato mbapo baada ya hapo barabara ya Kenya-Chambaani itafuatia.

Katika maelezo yake Mhandisi Mkaazi huyo alieleza kuwa kutokana na wananchi wengi kupata mafunzo juu ya ujenzi wa barara hatua hiyo imeweza kurahisisha ujenzi huo wa barabara ambapo hufanya kazi kwa makundi baada ya kupata utaalamu.

Masoud alisema kuwa utaalamu unaotumika wa Emulsion Treated Base (ETB) katika ujenzi wa barabara hizo kisiwani Pemba ambao hutumia lami baridi ni ujenzi wa mwanzo kwa nchi za Afrika za Mashariki na tayari nchi mbalimbali zimeomba kuja kisiwani Pemba kupata mafunzo zikiwemo Kenya, Msumbiji na nyenginezo

Kwa mujibu wa maelezo ya Mhandisi huyo ujenzi wa barabara hizo sita zilizomo katika Mradi huo unatarajiwa kukamilika Disemba mwaka 2011.

Barabara hizo zinajengwa na Idara ya Barabara chini ya ufadhili wa Serikali ya Norway hadi kumalizika kwake zitatumia zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 9.

Nao wananchi wa vijiji hivyo wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti walisifu juhudi za Rais Karume katika kuimarisha Maendeleo na uchumi wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Walieleza kuwa juhudi za Rais Karume za kuimarisha miundombinu ya barabara kisiwani Pemba ni mkombozi mkubwa wa uchumi na maendeleo ya nchi na wananchi wake kwani faida kubwa itapatikana baada ya kumaliza ujenzi wa barabara hizo a,mbapo wananchi watarahisishiwa kufanya biashara kwa uhakika, kuimarisha kilimo, uwekezaji, uvuvi na shughuli nyengunezo.

Katika ziara yake hiyo, Rais Karume alifuatana na viongozi mbali mbali akiwemo Mkewe Mama Shadya Karume.

Jioni ya leo Rais Karume anatarajiwa kujumuika na Waislamu na Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa ajili ya futari ya pamoja aliyowaandalia huko katika viwanja vya Ikulu ndogo ChakeChake Pemba.

No comments:

Post a Comment